Aya:
19
Mahali iliteremshwa:
Makka
SURAT AL- AA'LAA
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanza kwa kumtakasa huyo aliye umba vitu vyote, na akavifanya vyote sawa kwa kuvishughulikia, na akakadiria kila kitu kwa kinavyo silihi, basi akakiongoza kifikilie hivyo. Na akaotesha malisho ya wanyama, na khalafu akayafanya makavu yaliyo ingia weusi. Kisha Aya zikatoa khabari kwamba Mwenyezi Mungu atamsomesha Mtume wake Qur'ani, naye ataihifadhi, wala hatosahau chochote katika hivyo ila apende Mwenyezi Mungu. Na atamsahilishia kwa wepesi. Kisha Sura inamuamrisha Mtume akumbushe kwa Qur'ani apate kukumbuka mwenye kuogopa, na ajitenge na ukumbusho huyo mwovu atakaye ingia kwenye Moto mkubwa. Na Aya zimetilia mkazo kwamba uwokovu ni wa mwenye kujisafisha, na akalikumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akasali. Na Sura imekhitimisha kwa kubaini kwamba yaliyo kuja humu yamethibiti katika Vitabu vya zamani, Vitabu vya Ibrahimu na Musa.