Aya:
49
Mahali iliteremshwa:
Makka
SURAT ATT'UR
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanza kwa kiapo cha watano katika bora wa viumbe kuwa adhabu itawateremkia hao wanao kanusha. Kisha ikafikia kusimulia kuwateremkia hiyo adhabu, na namna zake mbali mbali siku ya kufufuliwa na kulipwa. Na ikaingia kutaja mazungumzo juu ya neema za wachamngu na watakayo stareheshwa nayo katika Mabustani ya milele, na namna ya ukarimu watakao upata, na kisha yatakavyo tua macho yao kwa kuwa dhuriya zao watavyo wafuata, na kunyanyuliwa vyeo vyao wawafikie wao. Na baada ya hayo Sura inamuamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. adumishe kukumbusha bila ya kujali wanayo mzulia makafiri kumpinga yeye, au kushughulika na wayasemayo juu ya Qur'ani tukufu, kwa vile inavyo onyesha kuwa wameshindwa kuleta maneno mfano wa Qur'ani.
Sura hii pia imekashifu maoni yao makafiri ya ufisadi ya kutangaza upotovu wao, na uovu wa kupima kwao. Kisha ikakhitimishia kwa kumuelekea Nabii s.a.w. na kumwambia awaachilie mbali mpaka watakapo ikuta siku yao watapo situshwa, naye akaamrishwa aistahamilie hukumu ya Mola wake Mlezi ya kuwapa muhula hao, kwani hayo hayatamdhuru kitu yeye kwa sababu yumo katika uhifadhi wa Mola wake Mlezi na ulinzi wake. Kadhaalika imemtaka amtakase Mwenyezi Mungu na katika nyakati zote, na katika kila msimamo atakao kuwamo kwa jambo lolote, na usiku zinapo tua nyota.